
Mkurugenzi wa Sekta Ofisi ya Rais Tamisemi, Dk Andrew Komba amesema uzinduzi wa mwongozo huo ni katika kueleka awamu ya pili ya kampeni hiyo itakayozinduliwa rasmi na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ifikapo Desemba 7 mjini Dodoma.
“Mwongozo huo utasimamia na kutekeleza shughuli zinazohusiana na mazingira na umelenga katika kutoa maelezo stahiki namna ambavyo vituo vya afya, ikiwemo ngazi za chini mpaka juu ili maelekezo hayo yaweze kutumika katika upangaji wa mipango na uandaaji wa bajeti zitakazotumika,” amesema Dk Komba.
Naye Mratibu wa Kampeni ya Kitaifa ya Usafi ya Mazingira, Anyitike Mwakitalima amesema kutokana na kulegalega katika baadhi ya maeneo, waligundua kwamba kisababishi kimojawapo ilikuwa ni ukosefu wa mwongozo wa taifa ambao wadau na serikali ingeutumia kusimamia usafi wa mazingira.
Aidha amesema malengo ya kitaifa ifikapo June 2021 ni kuhakikisha hakuna kaya isiyo na choo.
Mkurugenzi wa Mipango kutoka Shirika la Water Aid, Abel Duganga amesema kutokana na kukosekana kwa mwongozo huo unaopima hali ya maji nchini utendaji wa serikali na wadau ulikuwa ukisuasua, lakini sasa utawezesha kuwa na vigezo vinavyofanana katika kupima na kuwa na takwimu sahihi.