Alhamisi , 1st Dec , 2016

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema hadi kufikia sasa, serikali imekwishaipatia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto shilingi bilioni 40 kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba.

Waziri Mkuu baada ya kuwasili Jijini Arusha, akipokelewa na viongozi wa mkoa wa huo

 

Amesema hatua hiyo inalenga kupunguza changamoto ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba iliyokuwa inazikabili hospitali mbalimbali nchini.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Manyara aliposimama wilayani Babati akiwa njiani kwenda Mkoani Arusha kwa ziara ya kikazi ya siku saba inayotarajiwa kuanza kesho.

Amesema suala la dawa kwa sasa linaenda vizuri, hivyo amewataka viongozi wa mikoa kuhakikisha dawa na vifaa tiba vinavyopelekwa katika hospitali zao zinatumika kama ilivyokusudiwa.

“Suala la dawa linaenda vizuri sasa. Hakikisheni mnadhibiti mianya ya upotevu wa dawa kwenye hospitali zetu kwa kuwachukulia hatua za kisheria watumishi wa sekta ya afya wasiokuwa waaminifu,” amesema.

Aidha, Waziri Mkuu amewataka viongozi hao kuweka utaratibu wa kujenga hospitali ya rufaa ya mkoa pamoja na kuhamasisha wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili kuwawezesha kupata huduma ya matibabu bure kwa mwaka mzima.