Jumatatu , 22nd Jul , 2019

Baraza la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini (NEMC), limesitisha matumizi ya Bwawa la Tope Sumu katika mgodi wa dhahabu wa ACACIA North Mara uliopo Nyamongo wilayani Tarime mkoani Mara.

Maafisa wa Baraza la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini (NEMC) wakati wakikagua

Marufuku hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi mkuu NEMC, Dkt. Samwel Mafwenga kufuatia mgodi huo kukiuka sheria ya uhifadhi mazingira ya mwaka 2004 ambapo wanahatarisha Afya za wananchi wanaishi jirani na migodi.

''Bwawa hili limekuwa likimwaga kemikali ambazo zinaweza zikaleta athari kwa maisha ya mwanadamu na tumeamua kulifunga ili wajenge jingine na sisi kama NEMC na serikali afya ya mwanadamu ni msingi kuliko hata hizo pesa'', amesema Dkt. Samwel.

Uchenjuaji wa madini pamoja na utililishwaji wa maji yenye kemikali katika mgodi huo umetajwa kuathiri Afya za wananchi wanaoishi jirani na mgodi wa Acacia North Mara, hivyo NEMC imesitisha utililishaji wa maji mpaka pale mgodi huo utakapojenga bwawa lingine kwa ajili ya kuhifadhia tope sumu hizo.

Ukaguzi huo uliofanyika leo Julai 22, 2019 umehusisha viongozi mbalimbali wa serikali ikiwemo Baraza la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC, wataalamu kutoka ofisi ya mkemia mkuu wa seriklai, pamoja na Tume ya Madini.