Jumanne , 19th Sep , 2023

Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imeanzisha mfumo mpya wa manunuzi kidigitali  utakaosaidia kudhibiti rushwa, mchakato wa zabuni kuchelewa na kuongeza uwazi wa zabuni kwa wafanyabiashara wanaomba tenda  serikalini

Akizungumza na wanahabari mara baada ya kamati hiyo ya bunge kumaliza mafunzo hayo, Ofisa Mtendaji Mkuu PPRA, Eliakim Maswi amewataka wafanyabiashara wote kuomba zabuni kwa kutumia mfumo huo mpya kama wanataka kupata kazi za serikali.

"Tulikuwa na mfumo unaoitwa TANEPS ulikuwa inatumika kwasababu sheria ilikuwa inaruhusu kuwa unaweza kutumia TANEPS Unaweza ukwtumia manual watu walikuwa wanatumia mpaka mwisho ni asilimia 18 , maana yake asilimia 82 hizi walikuwa wanatumia nje ya mfumo" amesema Eliakim Maswi 

Aidha amesema taasisi zinazosimiwa na Msajili wa Hazina na Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, zinapaswa kuanza kutumia mfumo mpya kwa shughuli za ununuzi wa umma na kwamba itakapofika Oktoba Mosi mwaka huu taasisi nunuzi zote za serikali hazitaweza kutuma mialiko ya zabuni katika mfumo wa zamani wa TANePS.

"Tulikuwa na kipindi Cha miezi mitatu Cha mpito tarehe moja mwezi wa kumi wote lakini mpaka Sasa tumeshasajili taasisi zinazotumia 545." aliongeza Eliakim Maswi 

Awali Mwenyekiti wa kamati hiyo ya bunge, Daniel Sillo alisema ni jambo la kupongeza kwa serikali kutenga fedha kwa ajili ya kutengeneza mfumo huo kupitia vijana wa kitanzania ambao ni wabobezi wa katika fani hiyo.

"Mfumo uliokuwa zamani ulikuwa na changamoto nyingi  ikiwemo rushwa kwasababu ya baadhi ya watumishi wasio waaminifu lakini mfumo haukuwa na uwazi kwahyo huu utasaidia kudhibiti hayo yote." alisema Daniel Sillo 

Alisema asilimia 70 ya bajeti ya serikali inatumika kwenye ununuzi kwahiyo panapokuwepo na sheria na mifumo mizuri fedha za serikali zinatunusurika.

"Tunatarajia mfumo huu utaongeza uwazi katika ununuzi wa umma, usimamizi mzuri wa fedha za umma, kudhibiti vitendo vya rushwa, ufuatiliaji kukidhi sheria, uwajibikaji na udhibiti wa manunuzi" alisisitiza Daniel Sillo 

Mfumo huo uliobuniwa na kutengenezwa na watanzania wenyewe umeanza kufanya kazi Julai 1, mwaka huu ukichukua nafasi ya mfumo wa awali wa TANePS utakaokoma kufanya kazi itakapofika Oktoba 1, mwaka huu