Jumatano , 20th Jan , 2016

Serikali imeitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuongeza makusanyo yake kwa mwaka kutoka sh. Bilioni 600 ambazo walijipangia mpaka kufikia Trilioni 1 ili fedha zisaidie kutatua matatizo ya wananchi, kuliko kuacha zikipotea kwa uzembe

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania Aloyce Matei.

Akizungumza mkoani Mtwara baada ya kufanya ziara katika Bandari ya mkoani humo, Waziri wa Uchukuzi, Ujenzi na Mawasiliano, Mhe. Makame Mbarawa, amesema serikali ya awamu ya Tano imejikita katika kuhimiza uwajibikaji kwa watendaji, na haitokuwa na huruma kwa mtu yeyote atakayefanya kinyume na hayo.

Amesema, bandarini kuna udhaifu mkubwa ambao serikali haiwezi kuuvumilia na kwamba itaendelea kuchukua hatua mpaka pale itakapojiridhisha kuwa pamekaa vizuri hata ikibidi kubakiza wafanyakazi wachache kuliko kuwa nao wengi ambao hawaleti tija inayohitajika.

Kwa upande wake, meneja wa Bandari ya Mtwara, Prosper Kimaro, amesema miongoni mwa mipango waliojiwekea ni kuongeza Gati 4 katika Bandari hiyo ambapo kwa kuanzia wataanza kwa ujenzi wa Gati moja ambayo tayari mamlaka imeshaamua na ujenzi wake utatumia fedha za ndani.