Alhamisi , 16th Apr , 2015

Wizara ya maendeleo ya mifugo na uvuvi imewahimiza wafugaji kusajili mifugo yao ili iwe rahisi kwa serikali kujua idadi ya mifugo iliyopo na kufahamu mahitaji ikiwemo kumudu uagizaji wa madawa.

Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Dkt, Titus Kamani

Waziri wa maendeleo ya mifugo na uvuvi Dkt, Titus Kamani amesema hayo mjini Morogoro wakati akizungumza na wadau wa sekta ya nyama waliokutana kuelimishana na kuhamasishana juu ya sheria ya nyama ambapo amesema iwapo serikali itakuwa na takwimu sahihi na za kutosha watamudu upatikanaji wa madawa na masoko ya nje,

Dkt. Kamani amesema kuwa masoko ya kisasa wanunuzi hutaka kujua nyama ilikotoka huku akisisitiza jamii kuachana na fikra potofu kuwa serikali inasajili mifugo ili kuichukua.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Morogoro Dkt. Rajabu Rutengwe amesema bado nyama ya hapa nchini imeendelea kuuzwa ikiwa chini ya viwango na ile yenye viwango ikiuzwa kwa bei ya juu na kwamba ipo haja ya kuboresha mfumo mzima wa ufugaji ili kuboresha uchumi wa wafugaji pamoja na taifa kwa ujumla.