Jumatano , 6th Jan , 2016

Serikali imeanza kurejesha ardhi kubwa ambayo baadhi ya watu waliimiliki kwa muda mrefu bila kuiendeleza huku wananchi wengi wakikosa ardhi kwa ajili ya kufanyia maendeleo.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi (Mb), akisisitiza jambo, wakati alipokuwa anatoa maelekezo.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mh. William Lukuvi ametoa agizo la hekta 1800 za ardhi ya Kapunga, katika kijiji cha Kapunga Wilayani mbalali Mkoani Mbeya zirejeshwe kwa Wananchi baada ya muwekezaji aliyepewa ardhi hiyo kushindwa kuiendeleza.

Akiongea na wanakijiji wa kijiji hicho katika mkutano wa hadhara, waziri Lukuvi amesema kwa Rais aliahidi wakati wa kampeni zake kuwa wale walioshindwa kuendeleza ardhi walizopewa, serikali itarejesha kwa wananchi wa eneo husika kwa ajili ya kufanya maendeleo.

Waziri Lukuvi baada ya kusikiliza kero za wananchi wa kijiji cha Kapunga amesema Rais Magufuli ameamua kuzirejesha kwa wananchi hekta hizo 1800 baada ya mmiliki ya shamba la Kapunga Estate kumilikishwa kimakosa.