Jumanne , 1st Sep , 2020

Wafanyabiashara wa Nafaka hususani Mchele katika soko la Nafaka la Tandika jijini Dar es salaam, wamesema mchele kwasasa umejaaa katika maghala kutokana na Soko la ndani kuzidiwa uzalishaji.

Mchele ukiwa sokoni

Wafanyabiashara wa Mchele katika soko hilo wamesema kufungwa kwa mipaka ya nchi za jirani na Tanzania zimewafanya wakulima wote kutoka mikoani kuleta  mchele kwa wingi jijini hapa hali ambayo inachangia kushuka kwa Bei ya  bidhaa hiyo kwa sasa.

"Yaani sasa hivi Dar es salaam pamekuwa kama dampo la wakulima kuleta kila kitu, mchele wote wanaleta hapa kutokana na kwamba masoko ya Zambia, Uganda na nchi za Jirani hawaingii kununua bidhaa hii ndo maana soko letu limezidiwa", alisema Juma Chalaza Mfanyabiashara wa Jumla wa Mchele.

Wafanyabiashra hao wameeleza kuwa katika kipindi hiki soko la mchele huwa ni kubwa tofauti ilivyo kwa kipindi hiki walioomba serikali kuhakikisha inaendelea kufanya jitihada za makusudi ili kuwanusuru mitaji yao.

"Unajuwa hata tufanye nini serikali ndo baba kama kuna namna ya kufanya ifanye ili tupate unafuu na tuendelee kujiendesha kwa kuwa masuala ya kodi na tozo mbalimbali za kiserikali ziko pale pale", alisema Omary Mbao Mfanyabiashara Tandika. 

Kurundikana kwa bidhaa hiyo sokoni kunampa mlaji nafuu ya kupata bei nzuri inayoanzia shilingi 950 kwa kilo hadi kufikia 2500 lakini ikiacha maumivu kwa wakulima na wafanyabiashara ambao mipango yao ilikuwa kupata faida.