Jumamosi , 12th Sep , 2015

Serikali imetoa dola za Marekani 100,000 kama mchango wake kwa ajili ya msaada wa kisheria katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (ACHPR), ambayo makao makuu yake yapo mkoani hapa.

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiwahutubia wafanyakazi na viongozi wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu mjini Arusha

Akizungumza katika hafla fupi ya kumuaga iliyoandaliwa na mahakama hiyo jana, Rais Kikwete amesema anatoa kiasi hicho cha fedha kwa kutambua umuhimu wa mahakama hiyo kwa nchi za Afrika.

Amesema Tanzania inaunga mkono juhudi za mahakama hiyo katika kuendesha kesi zake na wanaahidi kuendelea kuheshimu mahakama hiyo, sababu wanaona mwanga mbele na hali ya baadaye ya mahakama hiyo inaleta matumaini.

Katika hafla hiyo pia Rais Kikwete amezindua kijarida chenye taarifa muhimu za msingi za mahakama hiyo kilichotafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ili kutoa nafasi na fursa kwa wananchi wengi wa kuelewa shughuli za mahakama hiyo.

Aidha amezitaka nchi nyingine za Afrika ambazo hazijaridhia sheria zao za kuitambua mahakama hiyo kufanya hivyo.

Naye Rais wa Mahakama hiyo (ACHPR), jaji mkuu mstaafu Ramadhan, amesema mchango wa Tanzania katika ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika, hauwezi kutiliwa shaka na upo wazi, kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 20 ya Mkataba wa Mahakama hiyo.

Akizungumzia namna watanzania wanavyonufaika na mahakama hiyo, amesema licha ya kutokuwa na kitabu chenye taarifa za msingi za mahakama kilichotafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili, watanzania wameweza kuitumia mahakama hiyo kupata huduma kwa kuwasilisha na kufungua mashauri mbalimbali wakiwemo watu binafsi na asasi zisizo za kiserikali.

Hadi sasa nchi 29 tu kati ya nchi 54 wanachama wa AU ndizo zimeridhia itifaki ya kuanzishwa kwa mahakama hiyo Juni 9, 1998 nchini Burkina Faso na kuanza kutumika Januari 25, 2004.