Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemhakikishia Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuwa serikali yake ya awamu ya tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo tayari kushirikiana na kuimarisha zaidi mahusiano kati ya Tanzania na Israel katika nyanja mbalimbali ili kuleta manufaa kwa pande zote.
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Israel hapa nchini mwenye makazi yake mjini Nairobi - Kenya Yahel Vilan, Ikulu jijini Dar es salaam.
Aidha, Rais Magufuli ameahidi kuwa Tanzania itahakikisha inaanzisha ubalozi wake nchini Israel haraka iwezekanavyo.
Kwa upande wake Balozi wa Israel hapa nchini Mhe. Yahel Vilan pamoja na kumpongeza Rais Magufuli kwa kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na uongozi wake katika kipindi kifupi cha miezi miwili tangu aingie madarakani amemhakikishia kuwa Israel itaendelea kushirikiana na Tanzania na ipo tayari kuimarisha zaidi mahusiano.
Balozi Vilan ametaja baadhi ya maeneo ya ushirikiano katika kiuchumi kuwa ni pamoja na Kilimo, Maji, Ufugaji wa Nyuki na Sayansi na Teknolojia huku akibainisha kuwa Israel imewaalika jumuiya ya wafanyabiashara wa Tanzania kushiriki katika kongamano la biashara kati ya Tanzania na Israel litakalofanyika mjini Tel Aviv nchini Israel, mwezi Septemba mwaka huu.
Balozi Vilan pia ameahidi kufikisha ujumbe wa Rais Magufuli kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na pia ameahidi kuanzisha ofisi ya kutoa huduma ya VISA hapa nchini haraka iwezekanavyo.
