Ijumaa , 17th Jun , 2016

Wizara wa Mambo ya Ndani ya Nchi imesema ipo katika hatua za mwisho za kuanzisha mahakama ya kijeshi katika Idara ya Uhamiaji ili kuweza kuwadhibiti watumishi

Wizara wa Mambo ya Ndani ya Nchi imesema ipo katika hatua za mwisho za kuanzisha mahakama ya kijeshi katika Idara ya Uhamiaji ili kuweza kuwadhibiti watumishi katika idara ya uhamiaji ambao wanakiuka utaratibu wa utoaji wa hati za kusafiria.

Akijibu swali kuhusiana na mkakati wa wizara hiyo kudhibiti uhalifu Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Hamadi Masauni amesema wizara hiyo kupitia idara ya uhamiaji itawachukulia hatua watumishi au waombaji wa hati wanaotumia njia za udanganyifu ikiwemo wanaopokea rushwa.

Mhe. Masauni ameongeza kuwa kutokana na kuwepo kwa tatizo la kughushiwa hati hizo wameweka mfumo wa kielektroniki ili kuweza kubaini udanganyifu huo pamoja na kufuta hati za kusafiria kwa watu ambao wamepatikana na hatia ya usafirishaji wa madawa ya kulevya.

Hatua hiyo imekuja baada ya kuulizwa swali na mbunge wa Viti Maalumu Halima Bulembo katika kufahamu serikali imejidhatiti vipi katika kudhibi mianya ya utoaji wa hati za kusafiria, ili kuepusha matukio ya kihalifu yanahusishwa na utolewaji wa hati hizo kiholela.