
Rai hiyo imetolewa na Mtafiti wa masuala ya kilimo cha kisasa Bwana Laurian Adolf Mchau, alipokuwa akiongea kwenye kipindi cha Super Mix kinachorushwa na East Africa Radio, kuhusu nini kifanyike ili kumvutia kijana kujiingiza kwenye kilimo cha kisasa.
Bwn. Mchau amesema vijana wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu kilimo cha kisasa, hivyo kuwafanya kukichukia kwa kuiona kama ni adhabu na si ajira kwao.
"Cha kwanza kabisa ni kumfanya kijana huyu kuanzia elimu ile ndogo ya awali, aweze kujifunza kwanza kilimo kinamsaidia yeye aweze kuishi, elimu hii ianze kwenye elimu ya msingi ya awali sio mpaka kijana huyu atoke akajifunze akiwa chuo kikuu, aanze katika msingi wa chini, tutangeneza vijana watakaopenda hiki kilimo, na watajua kuwa kuna mazao ya muda mfupi na muda mrefu, kwa hiyo wataingia kwenye soko na kutengeneza ajira", alisema Mchau.
Pia Mchau amesema serikali isitangaze tu kufufua viwanda na kuifanya nchi kuwa ya viwanda, bila kuangalia kilimo kwani ndio rasilimali muhimu kwa viwanda.
Amesema mazao ambayo ni ya biashara akitolea mfano kahawa na pareto, endapo yataboreshwa na kuzalishwa kwa wingi, yanaweza kupelekea kuwepo kwa viwanda vidogo vidogo vya kusindika, na kuuza bidhaa iliyo kamilika na sio ghafi.
"Ningependa sana tunaposema tutaongeza ajira za viwanda, lazima tuanze na kilimo, kwa mfano kuna mazao ya biashara kama kahawa, mkonge, pareto, ningependa sana mazao haya tusiyasafirishe kama rasilimali, tuyapeleke yakiwa yamekwishasindikwa kwenye soko, tuwe na viwanda vidogo vidogo ambavyo vitafanya tunapata materials mengine ambayo yatatusaidia kuboresha kilimo chetu, lakini tunapoipeleka kwa wenzetu tunapeleka aina nyingine ya material ambayo ingetukuzia kilimo chetu", alisema Mchau.
Pia Bwn. Mchau ametoa wito kwa vijana na kuwataka kutochukulia kilimo kama adhabu, ila wachukulie ni moja ya kazi kama zingine na kuwa wabunifu katika masuala ya kilimo.