Mkurugenzi wa Idara ya habari maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba
Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa habari maelezo na msemaji mkuu wa Serikali, Thobias Makoba, akiwa eneo la ajali Kariakoo na kusema kuwa eneo hilo kwa sasa linakabidhiwa kwa Serikali ya mkoa wa Dar es Salaam.
“Baada ya zoezi la kuokoa na kuondoa kifusi kumalizia leo Novemba26, 2024 kuanzia saa8 mchana Maduka yaliyokuwa yamefungwa na biashara zilizokuwa zimesitishwa zinaruhusiwa kufunguliwa isipokuwa eneo hili ilipotokea ajali kwani uchunguzi unaendelea kwenye eneo hili”, Thobias Makoba, Msemaji wa Serikali.
Kuhusu shutuma za mmiliki wa jengo lililoporomoka kukamatwa Makoba anatolea ufafanuzi.
“Ni kweli tumesikia taarifa nyingi sisi ni Serikali hatuwezi kushindwa na jambo lolote mmoja wa wamiliki tayari anashikiliwa na Jeshi la Polisi na waliobaki tutawakamata mahali popote waliło”, Thobias Makoba, Msemaji wa Serikali.
Wafanyabiashara wana lipi kuhusu tamko hili.
“Tunashukuru sana kwa Serikali kutufungulia Maduka ili tuweze kuendelea na biashara zetu Hali ilikuwa mbaya sana”, Godfrey Kileo, Mfanyabiashara Kariakoo
“Tunaipongeza Serikali kwa kumaliza zoezi kwenye eneo lile tunashukuru pia kwakuwa waneturuhusu kujerea kwenye biashara zetu Hali ilikuwa mbaya sana”, Tazani Kwai, Mfanyabiashara Kariakoo.
Hali ilikuwaje wakati maduka yakefungwa?
“Tumeathirika sana kiukweli kwanza tumepoteza pili tumeumia kiuchumi, wateja walikuwa wanapiga sana simu na hatukuwa na uwezo wa kuwahudumia”, Yasinta Tarimo, Mfanyabiashara Kariakoo.
“Tumezoea tutoke ndio tule sasa hizi siku zote tumeishi kwa mateso sana maana tulikuwa hatujui hatma yetu ni lini tutafungua maduka yetu”, Jackson Pascal, Mfanyabiashara KAriakoo.
Wateja nao wamekutana na usumbufu kiasi gani?
“Mtaa uliotokea ajali ndio mtaa tulikuwa tunanunua vitu Vya jumla Vya watoto kwahiyo tulikuwa tukija tunazunguka sana mbaya zaidi maduka mengi yamefungwa ilikuwa usumbufu sana, wakati mwingine Serikali iongeze kasi ya maokozi ii kuepukana na changamoto hii”, Raphael Mallya, Mnunuzi wa bidhaa.
Ikumbukwe ajali ya jengo kuporomoka ilitokea Novemba 16,24 mpaka sasa ni takribani siku 10 zimepita ambapo ni watu 29 wamefariki na kadhaa kujeruhiwa huku wawili wakiwa bado wanapatiwa matibabu.