Jumanne , 13th Oct , 2015

Serikali ijayo imetakiwa kutoa kipaumbele kikubwa katika kujenga mahusiano bora ya kimataifa hususani Afrika Mashariki, kwa kutenga bajeti ya kutosha katika wizara hiyo, ili kuweza kujenga hali nzuri ya kiuchumi hususani kwa vijana.

Rai hiyo imetolewa na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Shyrose Bhanji alipokuwa akiongea kwenye kipindi cha Super Mix kinachorushwa na East Africa Radio, na kueleza kwamba sekta hiyo ni muhimu sana na kupewa kipaumbele, kwani itabadilisha maisha ya vijana kwa kiasi kikubwa.

"Serikali ijayo, itoe kipaumbele kikubwa kwa kutenga fedha za kutosha kwa wizara ya Afrika Mashariki, kwa sababu hii ni wizara moja nyeti mno, ambayo ikipewa umuhimu unaostahili, kwa kweli maisha ya Watanzania au maisha ya vijana yanaweza yakabadilika kwa kiasi kikubwa, watu wanaweza wakajiajiri wenyewe kwa kupeleka bidhaa kwa nchi nyingine wanachama, tukifanya hivyo tutakuwa tumemsaidia huyu kijana", alisema Shyrose Bhanji.

Pia Shyrose Bhanji amesema wananchi wanatakiwa kufahamu kuwa serikali haiwezi kumfanyia mtu kila kitu, na kuwataka watu kujituma kwani nchi imeshatengeneza fursa mbali mbali.

"Unajua kuna jambo moja ambalo Watanzania vile vile tulifahamu, serikali haiwezi kumfanyia kila mtu kila kitu, lazima Watanzania tufanye kazi kwa bidii, tujitume kwa mfano kuna mazingira mazuri tu yapo, kuna mazingira ya kupata elimu, kuna scholership zinatolewa kuna nafasi za ajira katika hizi nchi wanachama, lakini watu jhawaandiki barua za maombi ya kazi", alisema Shyrose.

Pamoja na hayo Mbunge huyo kutoka Bunge la nchi wanachama wa Afrika Mashariki ameitaka serikali pia kuboresha wizara ya kazi, kwani ndiyo wizara pekee yenye uwezo wa kusaidia vijana kwenye tatizo la ajira.