
Rai hiyo imetolewa na Profesa na Mtafiti wa uchumi kutoka chuo kikuu cha Mzumbe Honest Ngowi, alipokuwa akiongea kwa njia ya simu kwenye kipindi cha Super mix kinachorushwa na East Africa Radio, kujadili kuhusu serikali ijayo itaboresha vipi mazingira ya ufugaji ili kumvutia kijana kujiingiza katika kilimo cha kisasa.
"kwa hali ilivyo sasa hivi upande wa vijana, kinachotakiwa ni kuweka mazingira ambayo yatawavutia waweze kuwekeza katika hiyo sekta, na kwa vijana wengi wanachotaka ni suala la upatikanaji wa vitendea kazi kama mitambo, pembejeo, mitaji suala la mikopo ya uhakika, suala la umwagiliaji, hawataki kile kilimo cha kubahatisha, wanataka kile cha uhakika kisiwe kama suruba iwe ni kama kazi yenye staa kama kazi nyingine", alisema Prof. Ngowi.
Pamoja na hayo Prof. Ngowi amegusia suala la kutoa elimu na kusema kwamba kuweka kwenye mitaala pekee haitoshi, hivyo kuna umuhimu wa kuwawezesha na kuwaboreshea mazingira ya kazi maafisa ugani waliopo, ili kuweza kuwafikia wananchi kwa wingi na kutoa elimu.
"Mtaala ikiwepo ni suluhu moja na haitoshi, bado wanahitaji huduma za afisa ugani, tatizo ni kwamba wale maafisa ugani wanawezeshwa vipi kwa maana ya vitendea kazi, ukienda wilayani humo atakwambia hana usafiri, hana posho, hana motisha, kwa hiyo suala la mitaala ndio lazima iwepo lakini haitoshelezi kwa sababu kuna wengi sana ambao wako nje ya shule, na majority wameshamaliza na wanahitaji hizi huduma", alisema Prof. Ngowi kwenye mazungumzo yake.
Pia Prof. Ngowi amesema serikali inatakiwa kupitia mapendekezo na tafiti zilizofanyika miaka ya nyuma, na kuyafanyia utekelezaji kwani tatizo kubwa linaloikabili sekta hiyo ni utekelezaji, na si kuanza kutafiti upya.