
Said Selemani
Selemani ambaye ni Mtaalam wa Teknolojia ya Habari (IT) amesomewa shtaka hilo leo Agosti 17, 2023, na Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Serikali, Martha Mwadenya mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya mkoa wa Mwanza, Stella Kiama.
Mshtakiwa (Selemani) katika kesi hiyo ya Jinai namba 126/2023 baada ya kusomewa shtaka hilo analodaiwa kulitenda kinyume na kifungu cha 225 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura namba 16 marejeo ya mwaka 2022, amekana kutenda kosa hilo.
Agosti 12, Mwaka huu, Jeshi la Polisi mkoani Mwanza lilitoa taarifa ya kumshikilia Selemani kwa kosa la kumchoma mpenzi wake kwa kisu maeneo mbalimbali ya mwili wake, kisha kujijeruhi tumboni kwa kutumia kisu hicho akiamini amemuua mpenzi kwa kile kinachodaiwa ni wivu wa mapenzi.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, SACP Wilbroad Mutafungwa alisema tukio hilo lilitokea Agosti 6, mwaka huu katika nyumba ya kulala wageni iitwayo The Citizen iliyopo Pasiansi wilayani Ilemela mkoani Mwanza.
Hata hivyo, Wakili Mwadenya amesema upelelezi wa kesi hiyo umekamilika hivyo akaiomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya mshtakiwa kuanza kusomewa maelezo ya awali ya shtaka linalomkabili.
Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Stella Kiama ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 31 mwaka huu itakapoitwa kwa ajili ya kusomwa maelezo ya awali, huku mshtakiwa akiendelea kuwa chini ya ulinzi Hospitalini hapo.