Alhamisi , 15th Feb , 2018

Kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe Morgan Tsvangirai, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo, akiwa nchini Afrika Kusini akipatiwa matibabu ya saratani akiwa na umri wa miaka 65.

Tsvangirai ambaye anajulikana kwa kuwa mpinzani mkubwa wa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Robert Mugabe, alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa saratani kwa muda mrefu, na hivi karibuni kuripotiwa kuwa hali yake haikuwa nzuri na ilihitaji matibabu ya umakini zaidi.

Wakati wa uhai wake na kujihusisha na masuala ya kisiasa, Tsvangirai alikutana na masahibu mbal;i mbali ikiwemo kupigwa, kushtakiwa na aliwahi pia kuwa waziri mkuu, lakini hakuwahi kushika wadhifa mkubwa aliokuwa akiupigania, wa kuwa Rais wa Zimbabwe.

Tsvangirai na Mugabe walikuwa hawapikiki chungu kimoja, huku Tsvangirai akimuita Mugabe dikteta na asiyefaa, na Mugabe akimtaja kama kibaraka wa wazungu asiyestahili kuwa na wadhifa wowote kwenye nchi hiyo, kwani atairudisha utumwani kwa kutumika na wazungu.