Rais Paul Kagame wa Rwanda, akiwa na mwenyeji wake Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania, wakati kiongozi huyo alipowasili kwa ajili ya mkutano wa wakuu wa nchi zinazounda ukanda wa maendeleo wa kati jijini Dar es Salaam leo.
Akizungumza katika siku ya mwisho ya mkutano wa kimataifa wa wakuu wa nchi hizo unaofanyika jijini Dar es Salaam, rais Kagame amesema ujenzi wa reli hiyo una umuhimu mkubwa kwa Rwanda ambayo sehemu kubwa ya mizigo yake inategemea nchi zilizo katika mwambao wa bahari ikiwemo Tanzania.
Rais Kagame amepata pia fursa ya kutembelea kitengo cha makontena katika bandari ya Dar es Salaam pamoja na Makao Makuu ya shirika la reli nchini TRL, ambapo amezindua safari ya treni kati ya Dar es Salaam na Kigali, kama ishara ya kubariki ujenzi wa reli hiyo aliyodai kuwa ina umuhimu mkubwa kwa Wanyarwanda.
Mapema jana, Rais wa Tanzania Dkt Jakaya Mrisho Kikwete, alisema kuna haja ya kuhakikisha kuwa uendelezaji wa miundombinu ya ukanda wa kati wa maendeleo, ulenge pia katika kuboresha ustawi wa maisha ya raia wa nchi hizo.
Kwa mujibu wa rais Kikwete, uendelezaji huo uangalie pia namna ya kuboresha mawasiliano na upatikanaji wa nishati ya uhakika, ambapo ameshauri umuhimu wa ushirikiano ambapo nchi yenye hazina kubwa ya nishati inaweza kusambaza na kuuza kwa nchi jirani, na hivyo hivyo kwa suala la mawasiliano.
Aidha, Rais Kikwete aliahidi azma ya Tanzania ya kupunguza vizuizi vya barabarani katika barabara kuu kati ya Dar es Salaam na nchi jirani za Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kutoka vizuizi zaidi ya kumi vilivyopo sasa hadi vizuizi vitatu.