Alhamisi , 11th Jul , 2024

Ripoti ya uchunguzi iliyofanywa na wataalamu wa miamba kutoka Taasisi ya Geolojia na utafiti wa madini Tanzania (GST), TANROADS, na Chuo Kikuu Dar es Salaam kutokana na Kipande cha barabara chenye urefu wa mita 50 kupata mipasuko mikubwa eneo la Busunzu, wilayani Kibondo, mkoani Kigoma.

Barabara iliyopata mipasuko mikubwa eneo la Busunzu, wilayani Kibondo, mkoani Kigoma mwezi Februari.

Ripoti hiyo imepokelewa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Innocent Bashungwa ambaye amewaagiza TANROADS kuhakikikisha wanafanya usanifu wa barabara kwenye maeneo korofi wakati wa mvua kwa kushirikiana na wataalamu wa miamba ili kubaini tabia za maeneo hayo na kuepuka changamoto zinazojitokeza.

“Nimepokea taarifa za kitaalamu na nimejionea zaidi ya mita 200 namna ambavyo majanga ya asili yaliyoathirika eneo hili, Serikali iliunda jopo la kufanya utafiti wa kina kuanzia mwezi Februari na tulichokigundua hapa sio makosa ya Mhandisi, sio upigaji kama watu wengine  walivyodhani”- amesema Bashungwa.

Diwani wa Kata ya Busunzu Wilayani Kibondo, Paul Ngomagi amesema hapo awali wananchi walikuwa wanaitumia barabara hiyo katika shughuli zao za kila siku ambapo walikuwa wakitumia dakika 45 kutokea Busunzu hadi Kibondo Mjini lakini baada ya kutokea changamoto hiyo eneo Hilo wananchi wamekuwa wakisubiria hatua za Serikali zitakazochukuliwa kurekebisha eneo hilo lililoporomoka.

Itakumbukwa mnamo mwezi Februari, 2024 Mkoani Kigoma katika mradi wa barabara ya  Mvugwe - Makutano ya Nduta palijitokeza  nyufa ndogondogo na baadae kipande cha barabara hiyo kuongezeka kutoka mita 50 hadi kufikia mita 200 na kuporomoka chini kına cha mita 15 kutoka usawa ilipojengwa awali.