Ijumaa , 23rd Sep , 2022

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla, amemuelekeza Mkandarasi wa kampuni ya Estim Construction Ltd, kuongeza kasi ya ujenzi na maboresho ya soko la Kariakoo likamilike kwa wakati ili wafanyabiashara wa Kariakoo wafanye biashara katika mazingira bora.

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla na Mkuu wa wilaya ya Ilala Ng'wilabuzu Ludigija, walipokagua ujenzi wa soko la Kariakoo

RC Makalla ametoa agizo hilo wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya ukarabati wa soko lililoungua na soko jipya Kariakoo, lenye urefu wa ghorofa 6 ambapo ujenzi unagharimu zaidi ya shilingi bilioni 26 huku akikiri kuridhishwa na maendeleo ya ukarabati huo.

RC Makalla amesema kukamilika kwa soko hilo itabadili mfumo wa uendeshaji biashara kwa kutoa wigo mpana wa kupokea wafanyabiashara wengi zaidi kutoka wafanyabiashara 600 mpaka kufikia wafanyabiashara zaidi ya 2,000.

Kuhusu suala la Kariakoo kufanya biashara saa 24 kama Rais Samia alivyoelekeza, RC Makalla amesema kikosi kazi kinaendelea kufanya tathmini kisha kitawasilisha taarifa kwa ajili ya utekelezaji.