Ijumaa , 9th Jul , 2021

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Amos Makalla amelielekeza Jeshi la Polisi kuhakikisha kuanzia sasa mabasi yote yanashusha na kupakia abiria kwenye kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli kilichopo Mbezi Louis.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Amos Makalla akizungumza na wananchi katika kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli kilichopo Mbezi Louis.

RC Makalla amesema hayo wakati alipotembelea kituo hicho na kusikiliza kero na changamoto mbalimbali za wafanyabiashara kituoni hapo, na kusema kuwa utaratibu wa sasa unatoa mwanya wa  usafirishaji wahamihaji haramu na bangi.

Amesema Serikali inatambua kituo kimoja pekee cha mabasi ambacho ni Mbezi na uwekezaji uliofanyika ni mkubwa hivyo hakuna maana kama kila mmiliki wa mabasi atakuwa na kituo chake cha kupakia na kushusha abiria.

Aidha, RC Makalla ameelekeza uongozi wa kituo hicho kuweka utaratibu wa baadhi ya mabasi kushusha abiria kwenye eneo la kulaza magari ambapo kuna banda la mamalishe ili kuchochea biashara za wafanyabiashara hao.

Wakati huo huo RC Makalla ametembelea Soko la Machinga lililopo pembezoni mwa Stendi hiyo na kuagiza wafanyabiashara wote wahamishiwe sokoni hapo na uchunguzi ufanyike kwa wale waliopatiwa vibanda kwa upendeleo na kujuana.

RC Makalla ameendelea na ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo pamoja na kusikiliza kero za wanachi aliyoianza tarehe 7/7/2021 ndani ya mkoa wa Dar es Salaama ambapo leo ametembelea stendi ya Magufuli kwa ajili ya kukagua ujenzi wa barabara ya kuingilia kwenye stendi hiyo.