Jumatano , 16th Aug , 2023

Rais wa Tanzania ameiagiza Wizara ya Mambo ya nje kuweka mfumo utakaoonesha kazi zote zinazofanywa na balozi za Tanzania katika mataifa mbalimbali, huku akihimiza matumizi ya TEHAMA katika kurahisisha na kuharakisha kazi.

Rais Dk. Samia ameyasema hayo leo Ikulu ya Chamwino Dodoma wakati wa hafla ya uapisho wa mabalozi walioteuliwa hivi karibuni huku akihimiza kuwa mabalozi kupata semina za mafunzo ya matumizi ya mifumo hiyo.

''Mabalozi wengine unawaona pale ambapo ujumbe wa Tanzania umekwenda kwenye nchi hiyo, anapokea wageni, anawasindikiza , au watanzania wafanye ukorofi ndio utaona ripoti ya Balozi, au unamuona siku za sherehe za kitaifa za nchi hiyo, lakini mengine hakuna, hakuna la maana linalotoka huko,“ Rais wa Tanzania Dk Samia.

Aidha Rais Dk. Amewataka Mabalozi kujifunza zaidi jinsi mataifa mengine yanavyofanya katika ukuaji wa uchumi wa mataifa yao, ili wahamishie ujuzi huo nchini Tanzania, kwani kazi yao sio kufanya uwakilishi tu wa Tanzania katika mataifa hao.

''Mtuambie wenzetu wamefanya uchawi gani kukua kiuchumi,na sisi tunakosa nini, tuna rasilimali hatuzitumii? au kitu gani, ila niseme ni wazi wenzetu wamepiga hatua kubwa sana licha ya kuwa sisi tumewazidi kwenye rasilimali diplomasia ya uchumi ifanye kazi hapa, tujiulize tuliachwa wapi?,'' 

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amehimiza mabalozi kuwa wazalendo, huku akisisitiza kulindwa kwa maslahi ya taifa letu.

''Tusisahau tunalinda maslahi ya taifa letu, na sisi kama Wizara ya Mambo ya Nje tutashirikiana na Balozi zote katika kufanikisha majukumu yetu,'' amesema Waziri Dk. Stergomena Tax