Alhamisi , 1st Dec , 2022

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesisitiza umuhimu wa kuzidisha elimu na kampeni kuhusu maambukizi ya UKIMWI kwani kumekuwa na ongezeko kubwa la maambukizi hasa kwa vijana wadogo

Rais Samia ametoa kauli hiyo mkoani Lindi katika maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani ambapo kitaifa yameadhimishwa mkoani humo

"Kuna maambukizi yanakuwa ya vijana wetu wa miaka 15 hadi 24, tusipozuia lile safari yetu itakuwa ndefu sana ya kutokomeza balaa hili, kwahiyo ni vyema tukaelekeza nguvu sana kwenye kampeni na elimu ya kusimamisha maambukizi"

Aidha Rais Samia amesisitiza umuhimu wa usawa ili kutokomeza ugonjwa huo ifikapo kwama 2030

"Kukosekana kwa usawa kunarudisha nyuma juhudi zetu za kutokomeza ugonjwa huu ifikapo mwaka 2030, hivyo ni muhimu tutumie maadhimisho haya tutafakari kwa kina na kuhakikisha tunaweka mikakati itakayoimarisha usawa"

Akizugumzia baadhi ya changamoto zilizopo mkoani Lindi ikiwemo suala la wanyama aina ya tembo kuvamia makazi ya watu Rais Samia amesema kumekuwa na changamoto kubwa inayotokana na wafugaji kuvamia katika maeneo ya wanyama hao 

"Wafugaji wameingia kwenye mapori yote, kwahiyo hata yale mapori ambayo tembo wamekuwa wakijificha yameingiliwa na wenyewe wametoka kuangalia makao mengine, lakini pia inawezekana jinsi tunavyotanua mashamba ya korosho na ufuta ndivyo tunavyosogea kwenye maeneo yao"

"Lindi huku kulikuwa hakuna ng'ombe, wamakonde wakiona ng'ombe walikuwa wanakimbia, sasa wafugaji wametoka walikotoka wamejaa tele Lindi, kwahiyo hata tembo waliopo Lindi hawakuwa wanajua ng'ombe hawajawahi kuwaona, kwahiyo wameona viumbe vigeni vimeingia na wenyewe wametoka, Wizara husika fanyeni kazi jambo hili" amesema Rais Samia