Alhamisi , 16th Mar , 2023

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan, amemteua aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Madawa ya Kulevya (DCEA) Gerald Kusaya, kuwa Katibu Tawala wa mkoa wa Rukwa.

Kushoto ni Ngussa Samike, ambaye ametenguliwa, katikati ni Gerald Kusaya RAS mpya Rukwa na kulia ni Ally Senga Gugu RAS mpya Dodoma

Taarifa ya uteuzi huo imetolewa hii leo Machi 16, 2023, na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Zuhura Yunus, ambapo pia amemteua Aretas James Lymo kuwa Kamishna wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini, akichukua nafasi ya Gerald Kusaya, aliyeteuliwa kuwa RAS Rukwa

Mwingine aliyeteuliwa ni Ally Senga Gugu kuwa Katibu Tawala mkoa wa Dodoma, na kabla ya uteuzi huo alikuwa ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara.

Aidha Rais Samia ametengua uteuzi wa aliyekuwa Katibu Tawala mkoa wa Lindi Ngussa Samike na kumteua Zuwena Omar Jiri ambaye alikuwa RAS mkoa wa Pwani. Samike atapangiwa kazi nyingine.