Jumatatu , 4th Apr , 2022

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amekubali ombi la Waziri wa Kilimo Hussein Bashe la kuomba pikipiki ambazo wamepewa maafisa ugani ziweze kuwa mali zao baada ya miaka miwili.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiteta jambo na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe

Rais Samia ameyasema hayo leo Aprili 4, 2022 alipokuwa akizungumza na maafisa ugani wa kilimo Jijini Dodoma katika hafla ya kuwakabidhi pikipiki 7000 kama sehemu ya kuwawezesha kufanya kazi vizuri.

Licha ya kukubali ombi hilo, amesema kuwa huduma watakayoitoa maafisa hao ndio itakuwa kipimo cha kupewa umiliki kamili wa pikipiki hizo baada ya miaka miwili huku akiwasisitiza maafisa hao kuleta mageuzi kwenye sekta ya kilimo nchini.

"Hilo ombi nimelikubali, lakini siyo iwe blanketi. Tutakwenda kuwapima kwa huduma mnayoitoa, kwahiyo tutawapatia pikipiki baada ya miaka miwili lakini kwa masharti hayo" - Rais Samia Suluhu Hassan

Aidha, Rais Samia ametoa wito kwa vijana wa Kitanzania kuingia kwenye sekta ya kilimo huku akiwaasa kwamba hawatajuta kuwekeza kwenye sekta ya kilimo.

"Niwaombe sana vijana wa Kitanzania, ingieni kwenye sekta hii. Hamtajuta, mtakwenda kutengeneza pesa halali mikononi mwenu. Na nikuombe sana Waziri, zile blocks mnazotengeneza, tengeni blocks kwaajili ya vijana"- Rais Samia Suluhu Hassan.