Jumatatu , 19th Jul , 2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha inayashughulia malalamiko yote yanayotolewa na Watanzania kuhusu tozo mpya za miamala ya simu zilizoanza kutumika Jula 15 mwaka huu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba, hii leo Julai 19, 2021, akitoa tammko la serikali akiwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dk. Faustine Ndugulile na kuwaomba Watanzania kuwa watulivu kwani serikali inafanyia kazi malalamiko yote.

"Mhe. Rais naye ameguswa na jambo hili, amesikia maoni ya Watanzania wote, na yeye ameshatoa maelekezo kwamba tuyafanyie kazi haya malalamiko ambayo wananchi wanayatoa, nitoe rai kwa wananchi wawe watulivu kwenye jambo hili," amesema Dkt. Nchemba

Aidha, ameongeza kwa kusema kuwa, "Nitoe rai kwa wale wote wenye nia mbaya ambao mara zote huwa wanapenda kupotosha ama kubadili maana halisi ya jambo lililokuwa limekusudiwa wasifanye hivyo, mambo ambayo ni ya kisheria, sheria ya nchi ziheshimiwe, yale ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi tutayafanyia kazi na yale ambayo tunatakiwa kuyafafanua tutafanua".