Alhamisi , 11th Jan , 2018

Rais wa Angola  João Lourenço, amemfukuza kazi mtoto wa rais wa zamani wa nchi hiyo José Eduardo dos Santos ambaye alikuwa Mkuu wa mfuko wa utajiri wa taifa hilo.

Rais  Lourenço alikaririwa akisema kwamba ameamua kumbadilisha José Filomeno dos Santos kufuatia tume ya ndani ya uchunguzi juu ya utawala wa mfuko huo huku kukiwa na taarifa kwamba dola bilioni 5 kutoka katika mfuko huo zimetumika katika hali tete tangu mwaka 2011 mfuko huo ulipoanzishwa.

Awali Novemba 15, Rais huyo alimfukuza kazi binti mkubwa wa rais huo wa zamani, Bi Isabel dos Santos kama mkuu wa kampuni ya mafuta ya serikali ya nchi ya Sonangol.

Aidha Rais huyo amemteuwa Waziri wa Zamani wa Fedha kuwa mwenyekiti wa bodi  ya mfuko huo (FSDEA) Carlos Alberto Lopes.

Mfuko huo umekuwa ukitajwa sana kufuatia tuhuma zilizovujishwa na gazeti la Paradise kwamba ulilipa fedha nyingi mamilioni ya dola ikiwa na malipo ya ada kwa mfanyabiashara ambaye anafanya kazi kwa karibu na José Filomeno.