Mwenyekiti wa CCM taifa Dkt Jakaya Kikwete akihutubia maelfu ya wakazi wa Songea waliofurika uwanja wa Majimaji kuhudhuria maadhimisho ya miaka 38 ya kuzaliwa chama hicho
Dkt Kikwete ametoa agizo hilo katika uwanja wa Majimaji mjini Songea ambapo zimefanyika sherehe za maadhimisho ya miaka 38 ya chama hicho.
Akimnukuu mwalimu Nyerere, amesema kuwa Rais wa Tanzania anaweza kutoka chama chochote lakini Rais bora ni lazima atoke CCM hivyo amewataka viongozi wa chama hicho kuhakikisha wanafanya mikutano na kuwatembelea wananchi ili kujua matatizo yao kama anavyofanya Katibu Mkuu wa Chama hicho Abdulrahman Kinana.
Aidha ameonya kuwa wana CCM wanatakiwa kutambua kuwa endapo CCM haitashinda, nchi itayumba na huenda CCM isibaki kama ilivyo, kwa hiyo ni jukumu lao kuhakikisha CCM inaendelea kubaki madarakani kwa kila jitihada.
Amewataka wawe makini wakati wa kuteua wagombea hususani katika nafasi ya urais ili wapate mgombea mwenye uwezo wa kuendelea kujenga umoja ndani ya chama na taifa kwa ujumla, na pia mwenye uwezo wa kuongoza Tanzania na watanzania wakamkubali.
“Msifanye makosa katika kupata mgombea, chagueni mgombea atakayekubalika na mwenye uwezo, hata kama yupo lakini hajajitokeza, siyo vibaya kumshawishi kama mimi nilivyoshawishiwa…” amesema Kikwete.
Amewataka viongozi wa chama hicho kuwashawishi wanachama wote kujiandikisha katika daftari la kupiga Kura kwa mfumo wa BVR ili waweze kushiriki uchaguzi huo wakiwa na vitambulisho vipya.
Amesema “Kwa mahesabu yaliyopo CCM ina wanachama zaidi ya Milion 6, tukiwaongeza na hao kama milioni 2 hivi, itakuwa million 8, tayari tutakuwa na mtaji wa Kura million 8 za kuanzia, na hao million 8 kila mmoja ana mpenzi, akimshawishi mpenzi wake kuipigia CCM tutakuwa na kura million 16, ambapo tutaweza kumshinda mtu yoyote……”
Ameongeza kuwa “CCM ni chama cha kuongoza dola, siyo chama cha michezo wala muziki, mambo ya muziki Kapten Komba anatosha, yupo na Diamond pia, wanatosha hao, lakini sisi tuhakikishe CCM inaendelea kuogoza dola”