Rais aagiza Walimu 6000 waajiriwe

Jumanne , 6th Apr , 2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu amewataka Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) kujaza nafasi za walimu zaidi ya 6000 wanaohitajika kutokana na walimu hao wengine kustaafu na wengine kufariki na nafasi zao hazijazibwa tena.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Rais Samia ametoa kauli leo baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali ambao aliwateuwa Aprili 4, 2021, miongoni mwa viongozi hao ni makatibu wakuu wa wizara na wakuu wa idara mbalimbali ambao amewataka wakachape kazi na kushughulika na mapungufu yaliyopo katika maeneo yao ya kazi.

Kuna mahitaji ya Walimu zaidi ya 6000, Utumishi mpo hapa naomba muajiri hao walimu wakatoe huduma kwa Watanzania hivyo basi Tamisemi na Utumishi mkashughulike na hilo mara moja”, amesema Rais Samia.

Ameongeza kuwa,  “Tamisemi mnajukumu kubwa la Elimu na Afya za Watanzania, mkasimamie miradi ya Elimu hasa Shule za Sekondari za Wasichana

Katika hatua nyingine Rais Samia amesema kuwa viongozi wa kitaifa wakikutana na mabango katika ziara zao, atawaondoa kazini mkurugenzi wa halmashauri na wakuu wa wilaya husika. Amesema imekuwa ni kawaida viongozi wakifanya ziara mikoani na wilayani wanapokewa na mabango ya wananchi wakilalamikia kero mbalimbali na masuala wanayolalamikia si ya kitaifa.

Tumezoea tunapokwenda kwenye ziara mikoani  na wilayani tunapokelewa na mabango ya wananchi wakilalamika kero mbalimbali, mabango yale mengine wala siyo mambo au masuala ya kushughulikwa katika ngazi za juu ni masuala ya kushughulikwa huko chini.”

Aidha Rais Samia ameongeza kuwa katika suala la ukusanyaji wa mapato,ameitaka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi)  kwenda kukusanya mapato na matumizi yafanywe kwa kufuata sheria na kanuni zilizopo.