Alhamisi , 16th Jun , 2016

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kamati za ulinzi na usalama nchini ili amani na mshikamano vizidi kutamalaki nchini.

Waziri mkuu ameyasema hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Singida Mjini Mussa Ramadhani Sima aliyetak kujua kwa nini wabunge wasijumuishwe katika kamati za ulinzi na usalama katika maeneo wanayotoka.

Akijibu swali hilo Waziri Mkuu amesema kwamba sheria inabainisha wazi kwamba wajumbe wanaotakiwa katika kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa na wilaya wapo kisheria hasa wakuu wa vyombo vya usalama.

Majaliwa amewataka wabunge kushirikiana na kamati za ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa ili kulinda nchi yetu na wakipata taarifa yoyote watoe katika vyombo hivyo.

Aidha Waziri Mkuu ametumia wasaa huo kutoa wito kwa wananchi kote nchini kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola wanapoona au kuhisi tukio lolote la uvunjifu wa amani ili kuhakikisha nchi inakuwa salama.