Prof. Ndalichako ahimiza elimu ya watu wazima 

Jumatano , 9th Jun , 2021

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, ameitaka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kutoa kipaumbele kwa elimu ya watu wazima ili kusaidia katika kuiboresha na kuinua.

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako

Prof. Ndalichako ametoa ombi hilo katika Kongamano la Kimataifa kuadhimisha miaka 50 ya elimu ya watu wazima Tanzania, ambapo amesema elimu ya watu wazima ni muhimu kwa nchi yetu.

"Kila Halmashauri tunakuwa na afisa elimu ya watu wazima, kuna baadhi ya maeneo elimu ya watu wazima imelala, kila mmoja ajitathimini katika halmashauri yake wanafanya nini na wanamipango gani kuhusu elimu ya watu wazima, naomba TAMISEMI katika mambo yote ya kipaumbele hebu twende na elimu ya watu wazima," amesma Prof. Ndalichako.

Aidha, Prof. Ndalichako amesema kuwa wataandika pendekezo kwa Waziri Mkuu kuhusu maafisa elimu ya watu wazima ambao hawafanyikazi.

"Tunapopokea taarifa, tupate pia na taarifa ya elimu ya watu wazima, vinginevyo Mhe. Waziri Mkuu tutaandika pendekezo maafisa elimu ya watu wazima ambao hawafanyi kazi tuwagawe bure katika maeneo mengine yanayohitaji watu wachapakazi," amesema Waziri Ndalichako.