Jumatano , 30th Dec , 2015

Makontena mengine 11884 pamoja na magari 2019 yamebainika kuwa yametolewa katika bandari ya Dar es salaam bila kufuata taratibu za ulipaji wa kodi na kulikosesha taifa mapato ya zaidi ya shilingi bilioni 49 na kuwataka wahusika walipe haraka.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof.Makame Mbarawa

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema hayo jana jijini Dar es salaam na kuongeza kuwa ukwepaji huo wa kodi ulifanywa na bandari kavu zinahusika na makontena na bandari kavu zinazohusika na uingizaji wa magari huku akiwataka waliolipa wawakilishe vielelezo vyao.

Prof. Mbarawa amesema kuwa kutokana na sakata hilo watumishi 7 wa mamlaka ya bandari wanaohusika na bandari kavu za makontena na magari wamekamatwa na kufikishwa katika vituo vya polisi kwa hatua zaidi za kisheria huku wengine nane wakitafutwa.

Desemba 7 mwaka huu waziri mkuu Kasim Majaliwa alitangaza upotevu wa makontena 2431 katika bandari kavu nne za Azam, DICD, JEFAG na PMM ambapo safari hii bandari kavu hizo nne zimehusika tena na upotevu na makontena hayo mengine.