Jumanne , 6th Dec , 2016

Mkazi wa  mtaa wa Mgombani katika mji mdogo wa Tunduma wilayani Mbozi mkoani Songwe amekutwa akiwa amefariki kutokana na kile kinachotajwa kuwa ni unywaji pombe kali kupita kiasi pasipo kula.

wakazi wa Tunduma wakiwa katika shughuli zao.

 

Kamanda wa Polisi mkoani Songwe Mathias Nyange alimtaja kijana aliyepoteza maisha katika tukio hilo kuwa ni Edimund Josephat (30).

Kamanda Nyange alisema kijana huyo alikutwa nyumbani kwake eneo la Mgombani kata ya Kaloleni mnamo Desemba nne mwaka huu saa tatu asubuhi akiwa amefariki dunia.

Kamanda huyo alisema ilithibitika kuwa kijana huyo alipoteza maisha kutokana na Unywaji pombe kali baada ya mwili wake kufanyiwa uchunguzi na madaktari na kubaini kuwa pia alikuwa hajala chakula.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe - Mathias Nyange

Hata hivyo Kamanda Nyange alisema bado haijabainikaa ni aina gani ya Pombe kali aliyokunywa hata ikapelekea umauti kijana huyo huku pia jeshi la polisi likiendelea na uchunguzi juu ya kifo hicho ikiwamo kufuatilia ni wapi alikokuwa akinywa pombe.

Aliwasihi vijana kuepuka pombe kali akisema licha ya kuzorotesha nguvu kazi ya taifa kwa kupunguza mchango wa nguvu kazi ya vijana kwenye shughuli za maendeleo,pia ni hatari kwa afya na maisha yao kwa ujumla.