Jeshi la polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam leo limetumia mabomu ya machozi kutawanya msafara wa mwenyekiti chama cha Wananchi CUF Profesa Ibrahim Lipumba, uliokuwa ukitokea Temeke jijini DSM kuelekea Mbagala Zakiem, ambako ulikuwa ufanyike mkutano maalum kwa ajili ya kumbukumbu ya wafuasi wa chama hicho waliofariki mwaka 2001 visiwani zanzibar.
Jeshi hilo limetumia nguvu kubwa kuwapiga waandishi wa habari waliokuwa wakitekeleza majukumu yao ambapo mwenyekiti wa taifa wa chama Profesa Ibrahim Lipumba na viongozi wengine wamejikuta wakipata kipigo na hatimaye kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi.
Awali polisi ilizuia wafuasi hao kufanya maandamano kutokea Temeke kuelekea mbagala na kuwataka waende bila maandamano, Professa Lipumba alitii amri hiyo na kutangaza kuahirisha mkutano huo.
Hali ya sintofahamu ilianzia katika ofisi CUF Temeke pale mwenyekii wao Profesa Lipumba alipowatangazia wafuasi hao kuwa hakutakuwepo na maandamano ya kuelekea katika viwanja wa Zakhem na badala yake atakwenda mwenyewe katika mkutano huo kuwatangazia wananchi ambao tayari walikuwa wameanza kukusanyika katika eneo la mkutano.
Baada ya tangazo hilo safari ikaanza na ndipo mvutano ukaanza baina ya polisi na viongozi wa CUF ambapo baada ya mabishano na majadilino ya muda mrefu safari ikaanza tena kutokea Temeke kuelekea Zakhem.
Baada ya hapo msafara wa Professa Lipumba ulianza kuelekea Mbagala Zakiem lakini walipofika maeneo ya Mtoni kwa Azizi Ally jeshi la Polisi lilizuia msafara huo na likatolewa agizo lingine la kusitishwa kwa msafara huo.
Baada ya majadiliano hayo hali ya hewa ikabadilika ambapo jeshi hilo lilianza kulipua mabomu ya machozi na kukawakamata wafuasi wa chama hicho huku likiwapa kichapo wakati wa kuwapakiza kwenye gari lao akiwemo Professa Lipumba.
Baadhi ya mabomu yaliyokuwa yanarushwa yalidondoka katika makazi ya watu likiwemo darasa dogo la wanafunzi wenye umri usozidi miaka mitano ambapo walionekana wakitokwa machozi huku mwalimu wao Bi Halima Semsela akidai kuna watoto wengine hajui walipokimbilia.
EATV imemtafuta Kamanda wa Polisi Kanda maalum ya DSM Kamishna Suleiman Kova lakini simu yake imepokelewa na msaidizi wake ambaye amedai kuwa Kamanda yupo kwenye kikao, pia Kamanda wa Polisi wa Polisi Mkoa wa Temeke ACP Kihenya M Kihenya ametafutwa lakini simu yake haikupatikana.