Ijumaa , 31st Jul , 2015

Jeshi la polisi nchini Tanzania limesema limejizatiti kwa kutoa mafunzo kwa polisi katika jitihada za kulinda amani na ulinzi kwa raia hususan katika kipindi cha uchaguzi mkuu.

Hayo yameelezwa leo jijini Dar es Salaam na Kamishna wa Polisi Msaidizi Mwandamizi (SACP) Mary Nzuki wakati wa kutoa vyeti vya kufuzu mafunzo yaliyotolewa na wakufunzi kutoka jeshi la polisi nchini Marekani ambapo amesema mafunzo hayo yameshirikisha zaidi ya polisi 90 ambapo yatasaidia katika kusimamia amani na kutetea haki za binadamu.

Aidha, Kamishna Nzuki amewataka raia kufuata taratibu na sheria zilizowekwa na kuwa kwa wale watakakwenda kinyume jeshi la polisi halitasita kuwashughulikia, na kutaka kutoa taarifa pale wanapoona kuna vitendo vya uhalifu na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo ni ya mwendelezo ambapo wanatarajia kuyatoa kwa askari wa jeshi la polisi nchi nzima ili kuweza kuwajenga kiasikolojia katika kusimamia makundi mbalimbali ya jamii haswa katika kipindi cha kampeni za wagombea na katika uchaguzi mkuu.