Alhamisi , 21st Aug , 2014

Mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Humphrey Pole Pole amependekeza bunge maalumu la Katiba liendelee lakini kwa kufuata ushauri wa watu wachache wenye busara za kunusuru mchakato huo.

Mjumbe wa Iliyokuw Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Humphrey Polepole.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na East Africa Radio, Polepole ametahadharisha kuwa iwapo busara chache zilizosalia hazitatumika kunusuru mchakato huo, basi bunge maalumu la katiba litakuwa limeandika historia mpya kwa kutumia kiasi kikubwa cha rasilimali katika kudhohofisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa mujibu wa Polepole, mchakato wa kutafuta katiba mpya ni wa maridhiano baina ya pande hasimu ambazo kila moja itakuwa tayari kupoteza baadhi ya maslahi yake.

Wakati huo huo, zaidi ya watoto milioni tatu nchini Tanzania ni yatima na wanaishi katika mazingira magumu ikiwa ni pamoja kuzurura mitaani pasipo uangalizi wa wazazi,kutokana na kupoteza wazazi wote wawili.

Mkurugenzi mkazi wa asasi inayohusika na malezi ya watoto yatima ya S.O.S Villages tawi la Tanzania Bw. Anatory Rugaimukamu, amesema hayo jana wakati akizungumzia harambee itakayoendeshwa na asasi hiyo kwa ajili ya kukusanya shilingi bilioni 1.2 zitakazotumika kutoa malezi kwa baadhi ya watoto yatima nchini.

Kwa mujibu wa Bw. Rugaimukamu, amesema kuna haja ya Watanzania kujitolea kuchangia harambee hiyo kama sehemu ya mchango utakaowawezesha watoto hao kupata haki zao za msingi ikiwemo elimu na malezi kama wanavyopata watoto wengine.