
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole.
Polepole ametoa kauli hiyo leo Jumapili Oktoba 7, 2018 kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter ambapo amesema mwaka 2018 ndio mwisho wa chaguzi ndogo za ubunge, wale watakaoshindwa kuhamia CCM wabaki walipo.
“Tumezingatia na tunaweka jitihada zetu zote katika kushughulika na utatuzi wa shida za watu wetu wa Tanzania. Mwaka 2018 ndiyo mwisho kwetu kufanya chaguzi ndogo za ubunge kwa wale wanaohama vyama vyao na kujiunga na CCM. Watakaoikosa raundi hii mbaki hukohuko tutakutana 2020”, ameandika Polepole.
Mapema leo kabla ya Polepole kutangaza maelekezo hayo mbunge wa Simanjiro (CHADEMA), James Ole Millya amejiunga na chama hicho leo na kupelekea hadi sasa jumla ya wabunge saba wa upinzani kuvihama vyama vyao na kujiunga na CCM.
Wabunge hao ni Maulid Mtulia (Kinondoni), Godwin Mollel (Siha), Julius Kalanga (Monduli), Mwita Waitara (Ukonga) ambapo wanne hao walipojiunga CCM walipitishwa kuwania ubunge na kuibuka na ushindi.
Wengine ni Zuberi Kuchauka (Liwale) ambaye pia amepitishwa na CCM kuwania ubunge katika jimbo hilo kwenye uchaguzi utakaofanyika Oktoba 13, 2018 na mwingine ni Marwa Chacha aliyekuwa mbunge wa Serengeti kwa tiketi ya CHADEMA.