Bunge la Katiba Tanzania
Baraza la vyama vya siasa nchini Tanzania limesema kwamba linakusudia kukutana hivi karibuni kujaribu kuwashawishi wafuasi wa kambi ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kurejea katika bunge maalumu la Katiba.
Mwenyekiti wa baraza hilo ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama cha APPT Maendeleo, Peter Kuga Mziray, ameyasema hayo leo na kufafanua kuwa hatua hiyo inalenga kuzikutanisha pande mbili zinazokinzana ndani ya bunge maalumu la Katiba.
Mkutano huo utazikutanisha pande zote hasimu ndani ya bunge hilo na kuteua msuluhishi atakayewezesha mchakato wa Katiba mpya kuendelea baada ya kuwepo kwa maridhiano ya pande zote.