Jumatano , 30th Apr , 2025

Serikali ya Pakistan imedai kuwa ina taarifa za kijasusi za kuaminika zinazoonyesha kuwa India inapanga kuanzisha shambulio la kijeshi dhidi ya Pakistan ndani ya saa 24 hadi 36 zijazo.

Taarifa hiyo imetolewa na Waziri wa Habari wa Pakistan, Attaullah Tarar, ambaye ameonya kuwa iwapo India itatekeleza mashambulizi hayo, Pakistan itatoa jibu la haraka, thabiti na lisilotetereka.

Kauli hii imejiri baada ya India kuishutumu Pakistan kwa kutoa msaada kwa wapiganaji wanaodaiwa kuhusika na shambulio lililotokea katika eneo la Kashmir linalosimamiwa na India, ambapo watalii 26 waliuawa wiki iliyopita.
Hata hivyo, Islamabad imekanusha vikali tuhuma hizo, ikizitaja kuwa ni za kupotosha na zisizo na msingi.

Tarar amesema kuwa India inalenga kutumia tukio hilo kama kisingizio cha kuhalalisha hatua ya kichokozi ya kijeshi, akiongeza kuwa Pakistan haitakubali uchokozi wa aina yoyote bila kutoa majibu ya kulinda uhuru na hadhi yake.
Katika hatua za hivi karibuni, mamlaka nchini India zimeripoti kufanya msako mkubwa eneo la Kashmir inayoongozwa na India, ambapo zaidi ya watu 1,500 wamekamatwa kwa mahojiano.

Idadi ya waliokamatwa inaendelea kuongezeka, ingawa takwimu kamili bado hazijawekwa wazi na serikali imebomoa nyumba za watu zaidi ya kumi wanaotuhumiwa kuwa wapiganaji.

Ripoti zinaonyesha kuwa angalau mmoja wa watu hao anahusishwa moja kwa moja na mshukiwa anayetajwa kuhusika na shambulio hilo.

Kashmir ni eneo lenye mzozo wa muda mrefu kati ya India na Pakistan, ambalo linadaiwa na mataifa yote mawili lakini kila upande unalishikilia kwa sehemu tu.

Tangu mwaka 1989, Kashmir inayodhibitiwa na India imekumbwa na uasi wa kutumia silaha dhidi ya mamlaka ya India, ambapo vikundi vya wapiganaji vimekuwa vikilenga majeshi ya usalama pamoja na raia.

Hadi sasa, India haijatangaza rasmi kundi lolote inalolituhumu kwa mashambulio ya Pahalgam.