Ijumaa , 28th Aug , 2020

IGP Mstaafu Balozi Ernest Mangu amesema kuwa amehitimisha safari yake katika utumishi wa Jeshi la Polisi Tanzania akiwa salama na ameliacha Jeshi hilo likiwa na mafanikio.

IGP Mstaafu Balozi Ernest Mangu akikagua moja ya kikosi ndani ya Jeshi la Polisi.

IGP mstaafu Mangu amesema hayo katika hafla ya kuagwa iliyofanyika katika Chuo cha Taaluma ya Polisi kilichopo Kurasini jijini Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani Christopher Kadio.

Balozi Mangu amesema kuwa hakupata changamoto kubwa kwenye uongozi wake, isipokuwa uchaguzi wa mwaka 2015 baada ya Mawaziri Wakuu wastaafu wawili kuhamia upinzani.

“Hakuna changamoto iliyoniteteresha katika uongozi wangu, ila kuna matukio makubwa ambayo hatukuyatarajia yalitokea katika Uchaguzi wa mwaka 2015 ambapo Mawaziri Wakuu Wastaafu wawili walihamia upinzani walisababisha mtikisiko kidogo ila tulimaliza salama”, amesema IGP Mangu.

Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro, ametoa pongezi kwa kiongozi huyo Mstaafu na kumshukuru kwa uongozi wake ambao ulimuibua yeye pia ambaye amekuwa mrithi wake.

IGP Mstaafu Mangu amelitumikia jeshi la Polisi kwa miaka 37, ambapo mwaka 2017 Rais Magufuli alimteua kuwa Balozi wa Tanzania nchini Rwanda.