Alhamisi , 8th Jan , 2015

Waziri Mkuu Mizengo Pinda amekanusaha tuhuma mbalimbali zinazotolewa dhidi yake kupitia mitandao ya kijamii kuwa anahusika na kashfa ya uingizaji wa sukari kutoka nje ya nchi ambayo inadaiwa kumpatia mabilioni ya fedha.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda

Pinda amesisitiza kuwa ikiwa vyombo vya sheria vitachunguza na kumtia hatiani yuko tayari kwa adhabu yoyote ikiwemo kufungwa gerezani.

Akiwahutubia wananchi wa maeneo mbalimbali ya mkoa wa Katavi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya kashaulili mjini Mpanda, waziri mkuu Mizengo Pinda amesema tuhuma hizo zinaenezwa na baadhi ya watu wakiwemo wapinzani wake kisiasa zikilenga kudhoofisha uongozi wake na juhudi za serikali kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanzania.

Pinda amesema angekuwa anapokea mabilioni hayo ya fedha vyombo vya dola visingelifumbia macho jambo hilo na angekuwa miongoni mwa matajiri wa Tanzania na kamwe asingeishi maisha ya kimasikini anayoishi hivi sasa.

Aidha waziri mkuu Mizengo Pinda amepuuza baadhi ya kauli zinazotolewa na baadhi ya watu kwamba yeye kama waziri mkuu hana maamuzi katika serikali na mara zote amekuwa mtu wa kulialia.

Amesisitiza kuwa kazi anayoifanya ni kubwa inayozingatia misingi ya utawala bora na ya maadili ya uongozi na kama kuna mapungufu ya kiutendaji wananchi ndio wanaoweza kupima na kutoa maamuzi.