Jumamosi , 5th Jan , 2019

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemuita Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi pamoja na Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri zote zinazozalisha nguzo za umeme katika mkoa huo kufika ofisini kwake ili waeleze sababu za kuzuia nguzo hizo zisitoke.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo, wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji Nyoni,  wilayani Mbinga akiwa katika siku ya tatu za ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma na kusema jambo hilo linakwamisha zoezi la usambazaji umeme.

Wanieleze kwa nini wanazuia nguzo, wakati wananchi wanasubiri kuunganishiwa huduma ya nishati ya umeme wao wanazuia nguzo wanasubiri posho, wanaidai serikali wakati ni wao ni sehemu ya serikali  tutakutana ofisini kwangu Januari 7, saa tano kamili asubuhi", amesema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu amesema hayo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi ambao walilalamikia kitendo cha kutofikishiwa huduma ya umeme katika maeneo yao kutokana na kukosekana kwa nguzo ambazo zimezuiwa kwa sababu ya wahusika wanaidai serikali posho.

Waziri Mkuu amesema viongozi wengine watakaokuwepo kwenye kikao hicho ni pamoja na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, Waziri wa nchi OR-TAMISEMI, Selemani Jafo, Wenyeviti wa halmashauri hizo zilizozuia nguzo ili wamueleze sababu za kuzuia nguzo hizo.