Jumapili , 14th Sep , 2025

Taifa hilo la Himalaya kwa sasa liko tayari kuingia kwenye uchaguzi wa Wabunge Machi 5, mwaka ujao, kwa mujibu wa ofisi ya Rais katika taarifa yake jana Jumamosi.

Siku mbili baada ya Shushila Karki kuchukua madaraka ya Nepal kama waziri mkuu wa muda wa nchi hiyo, polepole nchi hiyo imerejea katika hali ya kawaida kufuatia siku za maandamano ya ghasia yaliyoongozwa na vijana nchini humo maarufu kama Jen Z.

Habari za uteuzi wa Karki zimeungwa mkono na nchi jirani ya India, ambayo Waziri Mkuu wake Narendra Modi alitoa pongezi zake katika chapisho kwenye X. China haikujibu chochote licha ya kuhimiza utulivu wakati wa maandamano, ikitoa wito wa ulinzi wa raia na kufanya kazi ili kurejesha utulivu.

Mamlaka za Nepal zimeondoa amri ya kutotoka nje katika mji mkuu wa nchi hiyo na maeneo jirani jana  Jumamosi huku hali ya utulivu ikirejea kufuatia kuteuliwa kwa waziri mkuu wa kwanza mwanamke wa taifa hilo la Himalaya baada ya maandamano ya wiki hii ambayo yalisababisha vifo vya takriban watu 51 na kuondoa serikali iliyokuwepo baada ya waziri mkuu KP Sharma Oli kuachia madaraka.

Taifa hilo la Himalaya kwa sasa liko tayari kuingia kwenye uchaguzi wa Wabunge Machi 5, mwaka ujao, kwa mujibu wa ofisi ya Rais katika taarifa yake jana Jumamosi. Haya yanajiri wakati Rais wa Nepal Ramchandra Paudel akitoa wito kwa washikadau wote kushirikiana katika kuendesha uchaguzi huo wa wabunge mnamo Machi 5 mwaka ujao.

Waandamanaji wa Gen Z wamefanya mkesha kwa kuwasha mishumaa huko Boudhhanath Stupa huko Kathmandu kuwakumbuka waliopoteza maisha katika maandamano ya kupinga ufisadi dhidi ya serikali ya awali ya KP Sharma Oli.

Takriban watu 51, wakiwemo waandamanaji 21, wafungwa tisa, maafisa watatu wa polisi na wengine 18, waliuawa katika maandamano hayo tangu Jumatatu,kwa mujibu wa polisi. Takriban wafungwa 1,000 waliotoroka kutoka jela nyingi nchini walirejeshwa, lakini zaidi ya wengine 12,500 wakifanikiwa kutoroka, kulingana na polisi.

Hasira za waandamanaji wa Nepal kando na kuzuiliwa mitandao zilitokana na kuzorota kwa uchumi, huku vijana wengi wakiwa hawajaridhishwa na jinsi wanavyohangaika kujikimu wakati viongozi wa kisiasa na vizazi vyao wakifurahia maisha ya anasa.

Vijana wengi wa Gen Z na wengine walisema wamekatishwa tamaa na ukosefu wa ajira hasa vijijini jambo ambalo limepelekea mamilioni ya watu kutafuta kazi katika mataifa mengine ya Mashariki ya Kati pamoja na Korea Kusini na Malaysia.