Jumatatu , 10th Jan , 2022

Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Pius Msekwa, amesema somo pekee ambalo amelitoa Spika wa Bunge la 12 aliyejiuzulu Mhe. Job Ndugai ni kwamba kiongozi muadilifu lazima aachie ngazi anapoonekana kwamba amekataliwa na wale waliomweka kwenye uongozi.

Kushoto ni Spika Mstaafu wa Bunge Pius Msekwa na kulia ni Job Ndugai

Kauli hiyo ameitoa hii wakati akizungumza na East Africa TV na East Africa Radio digital, zikiwa zimepita siku chache tangu Job Ndugai, aiuzulu wadhifa wake wa Uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo Januari 6 mwaka huu.

"Somo peke yake alilolitoa Ndugai ni kwamba ukiwa kiongozi muadilifu ukikataliwa na waliokuchagua ondoka, using'ang'anie na mimi nampongeza kwa hilo, ameonesha mfano using'anga'anie cheo ambacho unawaongoza hawakutaki, usiwe kama Trump, hilo halikubaliki," amesema Spika Mstaafu  Msekwa.