
Viongozi wa CHADEMA wakiwa wameshika kitabu chenye sera za chama chao toleo la mwaka 2018.
kitatekeleza vipi sera hizo wakati hakina serikali?.
Www.eatv.tv imefanya mahojiano na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Vicent Mashinji, ili kutaka kufahamu namna ambavyo watatekeleza sera hizo wakiwa kama chama kikuu cha upinzani nchini, wakati kuna chama kingine madarakani.
Dkt. Mashinji amesema, sera hizo zitasaidia katika utengenezaji wa Ilani ya Uchaguzi itakayotumika mwaka 2020 ikiwa ni baada ya kuzunguka nchi nzima na kutoa elimu kwa wananchi kwakuwa falsafa ya chama hicho ni 'Nguvu ya Umma'.
“ Sisi tutatengeneza uchumi wa soko na tutatoa kipaumbele kwa sekta binafsi kuwa ndio wasimamizi wakuu wa uchumi, na kwa sera hizi tunajua CCM itabeza kwamba tutatekeleza vipi wakati hatuna serikali lakini tunachotaka sisi ni wananchi wajue kuwa ikiichagua CHADEMA itakwenda kuwafanyia kitu gani”, amesema Dkt. Mashinji.
Dkt. Mashinji ameongeza kuwa kutoa sera sasa hivi ni kuwafanya wananchi wasiwe na wasiwasi na CHADEMA, ili waanze kuzichambua mapema kwani utekelezaji wa sera huwa ni kazi ya Umma na wala si chama cha siasa.
"Maamuzi ya kila kitu hufanywa na wananchi vyama vya siasa huwa kazi yake ni kushawishi tu wananchi wavichague kwakuwa wao ndio wapiga kura na kuchagua wanayemtaka awaongoze kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania", amesema Dkt. Mashinji.
Septemba 25, 2018 Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilizindua kitabu cha sera za chama hicho toleo la mwaka 2018 kikiwa na sera 12 ambazo zimezungumzia namna ambavyo chama hicho kimejipanga kuinua maisha ya mtanzania.
Miongoni mwa vitu ambavyo sera hizo zimejikita ni masuala ya katiba, utawala bora, uchumi wa jamii, mazingira, mambo ya nje, elimu na sayansi, mambo ya siasa ya ndani, pamoja na uchumi wa vijijini
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo wa toleo hilo, Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa Freeman Mbowe amesema sera za chama hicho kimelenga kuinua uchumi wa mwananchi mmoja kama ilivyokua ikitamaniwa na mwalimu Julius Nyerere kupitia sera za ujamaa na hasa kupitia azimio la Arusha la mwaka 1967.
“Mwalimu Nyerere alisema sera za Chadema zilikua sera za kuinua maisha ya watanzania, kwa hiyo chama chetu sio chama cha kutafuta uhuru, bali sera zetu zimejikita zaidi kuhakikisha kila mtanzania anakua na maisha bora, sera hizi zimelenga maeneo 12 na tutaweza kuzifanyia marekebisho mara kwa mara pindi zitakapohitajika pia ni ruhusa kunakiliwa na vyama vingine.”