Ijumaa , 16th Feb , 2018

Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi Mwigulu Nchemba amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Simon Sirro na timu yake kufanya uchunguzi wa kina juu ya mauaji ya aliyekuwa Katibu wa CHADEMA Kata ya Hananasif Daniel John yaliyotokea Dar es salaam.

Waziri Nchemba ametoa maagizo hayo akiwa mkoani Kagera wilaya ya Muleba katika kata ya kasindaga wakati wa uzinduzi wa uandikishaji wa vitambulisho vya Taifa mkoani humo

Waziri Nchemba amelitaka jeshi la polisi kuchunguza kwa kina tukio hilo na kujua undani wake kisha  nikuwaambia wananchi nini kinachoendelea.

"Mataifa mengine mtu akiuwawa shighuli zote zinasimama, tusiweke haya mazoea ya watu wanapote potea kama mtu kapuliza dawa ya mbu, kama jambo la kawaida tu, wafanye uchunguzi kwa kina kujua nani amehusika na tukio hili". amesema Waziri Mwigulu

Ameongeza kusema kuwa maswala ya demokrasia huamuliwa kwa peni na karatasi na si kwa panga, rungu wala mkuki na kila mtu anayo haki ya kuwa katika chama chochote cha siasa nchini.

Katibu Daniel John aliuawa kwa kukatwa mapanga baada ya kuamriwa kuingia kwenye gari na baadaye mwili wake kuokotwa kwenye ufukwe wa 'Coco Beach' ukiwa umekatwa mapanga sehemu mbalimbali.