Akizundua mradi huo wilayani hapa, Kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru, Godfrey Mzava amempongeza Mkuu wa wilaya hiyo, Joshua Nassari pamoja na viongozi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini ( RUWASA ) Wilayani Magu kwa utekelezaji wa mradi huo.
Pia amepongeza taasisi za manunuzi kutoka halmashauri ya wilaya ya Magu kwa kuzingatia Mfumo mpya wa kielektroniki wa manunuzi ya Umma (National - e - Procurement System- Nest) katika kutekeleza mradi huo.
Ametoa wito kwa taasisi za manunuzi nchini kuzingatia mfumo huo kwani Serikali imeelekeza manunuzi yapite kwenye mfumo wa Nest ili kuweka uwajibikaji uwazi.
“Tangu kuanza kutumika kwa mfumo huo hakuna tena malalamiko. Mwenge unaendelea kuelekeza taasisi nunuzi zote kuwa ziweke taarifa zote kwenye mfumo kuanzia kumpata fundi au mkandarasi,” amesema.
Awali Mkuu wa wilaya hiyo, Joshua Nassari amesema ukarabati wa mradi huo ulianza kutekelezwa tarehe 12 Januari 2022 na kukamilika tarehe 12 Agosti 2022 chini ya mkandarasi PET COOPERATION CO. LTD.
Naye Mbunge wa Magu, Boniventura Kiswaga (CCM) amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuelekeza fedha za UVIKO-19 karika ujenzi wa miundombinu ya mradi ikiwa ni pamoja na tangi la maji lenye ujazo wa lita 200,000, vituo 10 vya kuchotea maji, mtandao wa bomba wenye urefu wa kilomita 12.7.
“Naomba kuchukua fursa hii kuishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa jitihada za uboreshaji na ujenzi wa miundombinu mipya ya maji kwa kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 - 2025 Ibara ya 100, sera ya maji ya mwaka 2002 na sheria ya maji namba 5 ya mwaka 2019 kwa vitendo,” amesema.