Ijumaa , 9th Mei , 2014

Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam, inakabiliwa na uhaba wa vipimo vya ugonjwa wa dengue, vipimo ambavyo vinapatikana kwa uchache katika kituo maalum cha Utafiti kilichojengwa kwa muda na taasisi ya Ifakara Health Institute.

Mbu ambaye anadaiwa kuambukiza homa hatari ya dengue.

East Africa televisheni imebaini hayo baada ya kushuhudia wagonjwa waliofika Hospitalini hapo kwa ajili ya kupata kipimo hicho na hatimaye kurudishwa kwa madai ya kwamba vipimo vimekwisha na kuwaagiza warudi Jumatatu.

Akizungumzia hali hiyo Daktari Kiongozi wa Idara ya Wagonjwa ya Nje wa hospitali hiyo ya Rufaa ya Mwananyamala Dk. Lupinda Lupinda amethibitisha uwepo wa uhaba wa vipimo hivyo na kwamba juhudi zinafanyika kuhakikisha kuwa uhaba huo unatatuliwa haraka.