Mvua iliyoambatana na upepo mkali iliyonyesha katika kata za Nguandua na Ambureni wilayani Arumeru mkoani Arusha imesababisha maafa makubwa yakiwemo ya kuharibu hekari 125 za migomba , kuezua nyumba na kuangusha idadi kubwa ya nguzo za umeme na wananchi wa zaidi ya kaya 500 wanahitaji msaada wa haraka ukiwemo wa chakula.
Baadhi ya wananchi waliopatwa na maafa hayo wamesema mvua hizo zilizoanza majira ya saa kumi jioni ya siku ya Jumapili zilinyesha kwa muda mfupi wa dakika zisizozidi 45 pia zimeangusha idadi ku bwa ya miti kubomoa nyumba na baadhi ya vyanzo vya maji na wameiomba serikali kuwasaidia.
Mkuu wa mkoa wa Arusha bw Felix Ntibenda na timu ya kitengo cha maafa amewatembelea wananchi hao na amemtaka mkuu wa wilaya kushirikiana na viongozi wa kata na vijiji kufanya tathimini na kutoa taarifa haraka ili serikali iweze kuchukua hatua .
Mkuu wa wilaya ya Arumeru Hasna Mwilima amesema hatua za awali zimeshachukuliwa ikiwemo ya kuwaarifu watendaji wa TANESCO kuzima umeme kazi ambayo meneja wa shirika hilo kituo cha Usariver amesema wameshaifanya na wanaendelea kusimamisha nguzo zilizoanguka .
Kufuatia maafa hayo mkuu wa mkoa Ntebenda amewataka wananchi wanaoishi mabondeni kuchukua tahadhari za kuwawezesha kuepukana na madhara yanayoweza kusababishwa na mvua zilizoanza kunyesha na pia amesisitiza umuhimu wa wananchi kutumia mvua hizi kupanda miti