Ijumaa , 8th Dec , 2017

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini, TMA imetoa tahadhari  ya mvua kubwa  zinazotarajiwa kunyesha kwa saa 24 katika maeneo mengi ya mikoa ya ukanda wa Pwani zikikadiliwa kuzidi milimita 50.

Taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo imesema kiwango cha uhakika wa mvua hiyo ni juu ya asilimia 80 kwenye mikoa ya Tanga, Pwani, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba.  

“Kutakuwa na mvua kubwa usiku wa leo kuamkia kesho, sababu ikiwa ni kuimarika kwa vyanzo vya mvua katika ukanda wa Pwani  ikiwemo mgandamizo wa bahari unaozalisha mvuke wenye kutengeneza mvua”, imeeleza taarifa ya TMA.

Hivyo mamlaka hiyo imetoa tahadhari kwa wakazi wa maeneo hayo yaliyotajwa na kushauriwa kuendelea kufuatilia taarifa  za mamlaka hiyo  pamoja na tahadhari zinazotolewa.

Mamlaka ya hali ya hewa nchini imeahidi kuendelea kufuatilia mwenendo wa hali hii na itatoa mrejesho kila itakapobidi kufanya hivyo ili kuepusha madhara yanayoweza kuepukika.